Kikwete mgeni rasmi Tamasha la Pasaka
Na Mwandishi Wetu; Tarehe: 14th March 2011
RAIS wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete atakuwa mgeni rasmi wa Tamasha la Pasaka litakalofanyika siku ya sikukuu ya Pasaka, Aprili 24 mwaka huu katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha la Pasaka ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Msama Promotions waandaaji wa tamasha hilo, Alex Msama ilieleza kuwa Rais tayari amethibitisha kuhudhuria.
Alisema Rais Kikwete amekubali kujumuika na wadau mbalimbali katika tamasha hilo la aina yake na kwamba litakuwa bora kuliko matamasha mengine yaliyopita.
Alimshukuru Rais Kikwete kwa kukubali mwaliko wao na kuongeza kuwa hiyo ni furaja kwa waandaaji pamoja na Wakristo wote kwa vile siku hiyo ni sikukuu ya Pasaka.
Kwa mujibu wa Msama kiasi cha fedha kitakachopatikana kwenye tamasha hilo kitatumika kuwasaidia waathirika wa mabomu ya Gongo la Mboto, Dar es Salaam.
Hata hivyo Msama alisema kwamba lengo la awali la kuwasomesha yatima na kuwasaidia mitaji ya biashara wanawake wajane bado lipo pale pale.
“Pamoja kwamba tutawasaidia waathirika wa mabomu pia, lile lengo letu kubwa la tamasha hili kuwasaidia kuwasomesha yatima na wajane lipo pale pale,” alisema.
Chanzo: Habari Leo
No comments:
Post a Comment