Audio ya Sinema ya Yesu Katika Kisukuma
  
Audio ya Sinema ya Yesu Katika Kiswahili

Thursday, March 17, 2011

MWAITEGE APANIA TAMASHA LA PASAKA

Mwaitege apania Tamasha la Pasaka
Thursday, 17 March 2011 09:53
Na Mwandishi Wetu, jijini

MWIMBAJI nyota wa muziki wa injili nchini, Bonny Mwaitege, amesema amejipanga vizuri kuhakikisha anafikisha neno la Mungu kwa njia ya muziki wakati wa Tamasha la Pasaka Aprili 24, mwaka huu kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam. Akizungumza na gazeti hili leo asubuhi, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Msama Promotions, Alex Msama, amesema mwimbaji huyo kutoka mkoani Mbeya, alithibitisha kushiriki tamasha hilo na kuahidi kutoa nyimbo mpya.

"Mambo yanazidi kuwa mazuri, sasa tumemaliza mazungumzo na Maitege, amekubali kupanda jukwaani Aprili 24, mwaka huu," amesema.

Msama amewataja waimbaji wengine nyota waliothibitisha kupanda jukwaani wakati wa Tamasha la pasaka ni Rose Muhando, Upendo Nkone, Anastazia Mukabwa na Pamela Wamarwa kutoka Kenya.

Amesema Rose, katika tamasha hilo atatumia nafasi hiyo kuwapa vitu vizuri watu watakaohudhuria tamasha hilo, tayari amekamilisha nyimbo tano mpya zitakazosikika katika tamasha hilo.

Msama amesema kwa upande wa Anastazia, yeye atatumia nafasi hiyo kuwaonesha ubora wa albamu yake ya Vua Kiatu, aliyoimba kwa kushirikiana na Rose Muhando.

Tamasha la Pasaka la mwaka huu litafanyika Aprili 24,  mwaka huu jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda mkoani Dodoma Aprili 25 na Shinyanga Aprili 26."Pamoja na kuwapata nyota hawa watano, bado tunafanya mazungumzo na wengine, tukikamilisha, tutawatangazia," amesema.

Albamu ya Vua Kiatu ina nyimbo nane ambazo ni Vua Kiatu uliobeba jina la albamu hiyo, Ee Mungu, Usiwe Manamba, Nzizilela, Nishike Mkono Bwana, Wanaokudharau na Mfalme.

Kwa mujibu wa Msama, tamasha la Pasaka la mwaka huu, lengo lake kubwa ni kukusanya fedha za kuwasaidia watoto yatima na mitaji ya wanawake wajane.Pia, fedha zitakazopatikana katika tamasha hilo zitatumika kuwasaidia waathirika wa mabomu yaliyotokea katika kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Gongo la Mboto, Dar es Salaam.

Tamasha la Pasaka la mwaka huu litashirikisha waimbaji wa nyimbo za injili kutoka nchi sita ambazo ni Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Afrika Kusini na Zambia.

Chanzo: Dar Leo

1 comment:

Unknown said...

Asante kwa kazi kubwa mwafanya kutupa habari kuhusu huduma ya nyimbo Tz.Je asie mtanzania apate neema yakuwekwa kwa blog hii vipi?sisi ni ORIONI CHOIR kutoka D.R.Congo.Tafadhali mutusaidie vile kujulikana kimataifa.munaweza kutusikiliza kwenye www.orionichoir.skyrock.com kwa zimbo JINA LA YESU.E-mail yetu ni orionichoir_cbcabbo@yahoo.fr na orionichoir@gmail.com.
tutafurahi kupata jibu please.