Audio ya Sinema ya Yesu Katika Kisukuma
  
Audio ya Sinema ya Yesu Katika Kiswahili

Thursday, February 11, 2010

HATIMAYE MCHUNGAJI DR. HERRY MHANDO AREJEA KWA WASABATO

Baada ya kujitenga na kanisa, naona mtumishi huyu wa Bwana ameamua kurudi kundini. Soma habari kamili hapa chini.

Mwinjilisti Mhando arejea kwa Wasabato

Chanzo: Tanzania Daima (3/2/2010)

Mwinjilisti wa Kimataifa aliyeanzisha mikutano mikubwa ya mahubiri ya kila mwaka katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam, Dk. Herry Mhando, amerejea katika kanisa lake la awali la Waadventista Wasabato (SDA) nchini Tanzania alilojitoa mwaka mmoja uliopita.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dk. Mhando alisema ameiacha rasmi huduma yake ya kujitegemea ya Uinjilisti na maombezi aliyoianzisha inayoitwa Seventh-day International Ministry (Huduma ya Kimataifa ya Wasabato) iliyovuta waumini wengi wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo na kuamua kurudi kwa Waadventista Wasabato.

“Huu sio uamuzi wangu binafsi. Ila ni uamuzi uliotoka kwa Mwenyezi Mungu, kwani tangu nilipoanzisha huduma hiyo nimefanya maombi ya kufunga kwa siku 415 mfululizo, nikila mlo mmoja tu wa jioni.

“Roho wa Mungu akanielekeza kurejea nilikotoka, kule kwenye asili ya imani yangu ambako nililelewa vizuri ikiwemo kupata elimu yangu yote,” alisema Dk. Mhando.

Alipoulizwa kama uongozi wa makao makuu ya Kanisa la Waadventista wa Sabato, una taarifa yoyote juu ya maamuzi yake hayo, alijibu kuwa tayari ameshaujulisha kupitia Askofu Mkuu wake, Mchungaji Joshua Kajula, na wanaendelea kushangilizwa na taarifa hiyo.

Dk. Mhando alianza kufanya mikutano ya mahubiri ya wazi jijini Dar es Salaam iliyokuwa na mvuto mkubwa mwaka 1994 (viwanja vya Mnazi Mmoja) akitokea masomoni nchini Marekani na baadaye viwanja vya Jangwani katika miaka ya 1998, 2002, na 2006. Aliwahi pia kufanya mkutano maalumu wa kuombea Uchaguzi Mkuu katika Ukumbi wa Diamond Jubilee mwaka 2005.

Mwinjilisti Mhando amewahi kufanya mikutano mingine mikubwa katika bara la Afrika huko Kenya, Afrika Kusini, Zimbabwe, Uganda, DRC, Nigeria, Zambia, Namibia, Botswana, Malawi na Burundi. Nchi za Ulaya ni Uingereza, Uholanzi, Uswisi na Urusi. Mashariki ya mbali ni India na Ufilipino. Aidha, Marekani na Canada nako amewahi kuhubiri mara nyingi.

Dk. Mhando aliwahi kuwa mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu wa Kanisa la Waadventista Wasabato katika Jimbo la Kaskazini Mashariki mwa Tanzania (makao yake mjini Same) na Makao Makuu ya Kanisa hilo nchini (mjini Arusha) mwanzoni mwa miaka ya tisini kabla ya kwenda masomoni nchini Marekani.

No comments: