Audio ya Sinema ya Yesu Katika Kisukuma
  
Audio ya Sinema ya Yesu Katika Kiswahili
Showing posts with label HABARI. Show all posts
Showing posts with label HABARI. Show all posts

Wednesday, November 16, 2011

Habari: Martha Mwaipaja Achumbiwa

Na Gladness Mallya

Mwimbaji wa muziki wa Injili nchini, Martha Esau Mwaipaja (pichani)  amechumbiwa na Mchungaji, John Said anayehudumia Kanisa la Udhihirisho wa Injili lililopo Ukonga jijini Dar es Salaam, Risasi Jumamosi linakupa habari kamili.

Habari zisizo na chenga zilizotua kwenye meza ya gazeti hili juzikati zilisema, Martha atavishwa pete ya uchumba na mchungaji huyo kesho saa 6:00 mchana katika Kanisa la Victoria lililopo Ubungo External jijini Dar.

“Martha anavishwa pete ya uchumba Jumapili (kesho) na Mchungaji, John Said na baada ya zoezi hilo kutakuwa na sherehe ndogo kanisani hapo kwa ajili ya kumpongeza kwa kufikia hatua hiyo,” alisema mtoa habari ambaye hakutaka jina lake lichorwe gazetini.

Alipotafutwa kuzungumuzia suala hilo, Martha alikiri kuchumbiwa na mchungaji huyo na kuongeza shughuli ya kesho itanogeshwa na waimbaji wenzake kama vile Bahati Bukuku, Sarah Mvungi, Ambwene Mwasongwe na Christina Mwang’onda.

Wengine ni David Robert, Debora John, Josephine Mwasulama, Ado November, Jennifer Mgendi, Lianga George, Stella Swai na wengineo.
Chanzo: Risasi (Novemba 12-14)

Tuesday, September 13, 2011

Christina Shusho: Gwiji wa Injili Anayepasua Anga za Kimataifa

CHRISTINA SHUSHO: Gwiji wa Injili Anayepasua Anga za Kimataifa
Na Angela Semaya; Tarehe 7 Septemba 2011 

“UNIKUMBUKE Babaa unapowazuru wengine naomba unikumbuke, usinipite Yesu unapowazuru wengine naomba unikumbuke, unikumbuke babaa unapowazuru wengine naomba unikumbuke…”

Haya ni baadhi ya maneno yaliyomo katika moja ya nyimbo zinazomtambulisha vyema Mwimbaji wa Nyimbo za Injili, Christina Shusho.

Shusho amefanikiwa kujijengea sifa kwa mashabiki wa nyimbo za Injili ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kutokana na nyimbo zake kubeba ujumbe mzito kwa jamii, lakini ukiwa katika msingi wa neno la Mungu ambalo analiamini.

Umahiri wake katika kuimba nyimbo za Injili umemuwezesha Shusho kutambulika vyema na kujinyakulia Tuzo mbalimbali ikiwemo Tuzo aliyopata wiki chache zilizopita huko Nairobi, Kenya.

Shusho alikuwa kati ya wasanii wa Tanzania waliopata Tuzo za Muziki za Afrika Mashariki na Kati (EMAS) zilizofanyika Agosti 20, mwaka huu na kushirikisha wasanii mbalimbali wa kutoka nchi nane za Afrika Mashariki na Kati.

Mwimbaji huyo aliibuka na Tuzo ya Msanii Bora wa Kike wa Nyimbo za Injili akiingia na wimbo wake Unikumbe na kumshinda mwimbaji mwenzake kutoka Tanzania Upendo Nkone aliyeingia na wimbo wake Haleluya Usifiwe, Alice Kamande kutoka Kenya na wimbo wake Upendo na Gaby kutoka Rwanda na wimbo wake Amahoro.

Wasanii wengine wa Tanzania walioshinda Tuzo hizo ni Bendi ya Muziki wa Dansi ya Msondo, Ambwene Yesaya `AY’ na Khamis Mwinjuma `Mwana FA’. Kutokana na ushindi huo, HABARILEO Jumapili lilipata fursa ya kukutana na kuzungumza na Shusho kuhusiana na ushindi huo, kazi yake, maisha yake na mafanikio aliyopata kutokana na uimbaji wake wa muziki wa Injili.

Akizungumzia Tuzo hiyo, Shusho ambaye ni mama wa watoto watatu anasema ni heshima kubwa kwa Mungu na kwake hasa kwa kuwa alishindanishwa na wanamuziki wenye vipaji vikubwa vya uimbaji wa nyimbo za Injili akiwemo mwimbaji mwenyeji Alice.

“Kidogo nilipata hisia za woga iwapo nitashinda hasa kutokana na ushiriki wa Alice ambaye ni mwimbaji mzuri wa nyimbo za Injili, lakini pia shindano lilifanyika nchini kwao hivyo mashabiki wake nilihisi kuwa ni wengi zaidi, lakini Mungu ni mwema nikapata mimi hiyo Tuzo hivyo nina kila sababu ya kumshukuru Mungu,” anasema.

Shusho anasema ushindi huo umemfanya ajisikie kumheshimu na kumnyenyekea zaidi Mungu kwa kumpeleka kila hatua, lakini pia anaona fahari kuwa watu ndani na nje ya mipaka ya Tanzania wanatambua kipaji chake na kazi aliyopewa.

“Naona ushindi huu mbali na kumheshimu Mungu zaidi, lakini pia naona nimepewa jukumu zaidi kwa maana kukitumia kipaji changu nilichopewa kwa kuimba zaidi ya hapa na kufikisha ujumbe kwa jamii kupitia uimbaji wa Injili,” anasema.

Nini msingi au chanzo cha uimbaji wake? Shusho anasema msingi wake umeanzia nyumbani kwa kile alichoeleza kuzaliwa katika familia ya Kikristo ambayo ilipenda kuomba na kusali. “Mimi nimezaliwa katika familia ya kikristo, kwa hiyo Jumapili nilikuwa nikihudhuria Shule ya Jumapili (Sunday School) ambapo watoto tulikuwa tukifundishwa dini, na huko ndipo nilianza kuimba,” anasema.

Anasema alipokuwa akiendelea kukua alijiona kuwa na wito na akaona ajaribu kuimba mwenyewe na kugundua ana kipaji na wito wa kuimba nyimbo za Injili, hivyo alianza kutunga nyimbo zake. “Mwaka 2003/2004 niliamua kuingia Studio.

Baada ya kupata msukumo hasa 2004 nilitengeneza muziki na kuingia studio…unajua nilipoamua tu nikaanza kutunga nyimbo zangu, kwa hiyo niliingia studio na nyimbo zangu mwenyewe,” anasema. Shusho anasema msingi mkubwa wa nyimbo zake ni neno la Mungu.

”Hata kama nitatoa wimbo kwa ajili ya jamii, lakini lazima msingi wake uanze na neno la Mungu.” Kwa mujibu wa mwimbaji huyo, mtindo wa nyimbo wake ni kusifu na kuabudu na kwamba hatungi wimbo kwa msingi wa kumjibu ama kumshambulia mtu zaidi ya kumsifu Mungu kwa ukuu wake.

“Unajua kuna wengine wanaimba nyimbo za Injili, lakini ukiusikiliza uko katika hali ya ama kumjibu mtu au kumshambulia mtu baada ya kuapa jambo fulani. Mimi ni tofauti naimba kumsifu na kumuabudu Mungu,” anasema.

Hadi sasa Shusho ameshatoa Albamu nne ambazo ni Kitu Gani yenye nyimbo nane iliyotoka mwaka 2004/2005, Unikumbuke yenye nyimbo nane iliyotoka mwaka 2007/2008, Nipe Macho yenye nyimbo 10 na Kwa Kanisa la Kristo yenye nyimbo nane ambazo amezitoa pamoja mwaka 2010/2011.

Kwa mujibu wa Shusho, albamu ya Unikumbuke ambayo alizindua rasmi Novemba 30, 2008 ndiyo iliyomtambulisha vyema kwa mashabiki wa muziki wa Injili na hadi sasa ameendelea kufanya vizuri hadi sasa.

Akizungumzia kukua kwa muziki huo anasema muziki wa Injili umekuwa, kwa kile alichoeleza kuwa zamani kwaya ndio zilikuwa zikijulikana lakini tofauti na sasa nyimbo za Injili zimepenya na unakuta zikitambulika katika matamasha na mashindano makubwa ya nyimbo za Injili.

Shusho anasema kuimba kwake nyimbo za Injili kumemuwezesha kupata faida mbalimbali, lakini kwanza jamii kumtambua na kukifahamu kipaji alichonacho, pili kazi zake kutambulika na kukubalika, tatu anajiona kutumika vizuri na kwamba anaamini Mungu anaona anavyofanya vyema kazi yake na nne imemuwezesha kufahamika ndani na nje. “Mungu amenipa maono na mambo ya mbeleni.

Kwa kweli Mungu amekuwa akinibariki kwa njia moja au nyingine,” anasema. Kutokana na uimbaji wake wa nyimbo za Injili Shusho anasema ameweza kushiriki matamasha ya ndani, lakini pia katika nchi za nje ikiwemo Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uingereza.

Mbali na Tuzo ya EMAS ambayo ameipata wiki chache zilizopita lakini pia anasema ameshawahi kupata Tuzo nyingine ikiwemo Tuzo ya Meya Cup iliyotolewa nchini Kenya, Tuzo za Muziki wa Injili (Gospel Music Awards) iliyotolewa hapa nchini ambapo aliibuka mshindi wa Msanii Bora wa Muziki wa Injili na Tuzo ya Kenya Groove Music Awards ambapo aliibuka na Tuzo ya Msanii Bora wa Nje.

Akizungumzia mtindo wa muziki wa Injili hivi sasa anasema, “kila mtu amepewa staili yake ya uimbaji…lakini tunapaswa kukumbuka kila watu wana utamaduni wao kwa hiyo ni vyema tukaimba kuzingatia mazingira yetu. Mungu angefurahi zaidi kama Watanzania tutaimba kwa kuzingatia utamaduni wetu…sidhani kama Mungu asingependa tuimbe kama Wachina, au Wazungu na kadhalika, Mungu atajali tukiimba kwa namna na kipawa alichotupa.”

Anawashukuru mashabiki wake kwa kile anachosema wamemsaidia kwa ushauri wa aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumpa mapendekezo na kwamba wamemshauri abakie na staili yake ya kuimba kwa taratibu.

“Kama nilivyosema nyimbo zangu ziko kwa mtindo wa kusifu na kuabudu ndio maana naimba taratibu na hivyo ni rahisi mtu kusikiliza nyimbo zangu hata akiwa anasikiliza katika redio wakati anaendesha gari njiani au amerudi nyumbani anataka kutulia lakini akisikiliza nyimbo za Injili…mimi najiamini na naamini staili yangu ni njema zaidi na ndio nadhani naimudu,” anasema na kuongeza lengo lake ni kuliimbia kanisa ambalo litaendelea kuwepo milele.

Mbali na kuwa mwimbaji wa nyimbo za Injili, Shusho anasema anapenda kupendeza na kuonekana maridadi na ndio maana pia anajishughulisha na masuala ya ubunifu wa mavazi na pia ananunua bidhaa au vitu kutoka nje.

Lakini pia Shusho ni mtangazaji wa kituo cha televisheni SIBUKA na akiendesha kipindi kinachojulikana kama Gospel Hits.

Hata hivyo anasema lengo lake ni kuanzisha kipindi chake cha televisheni ambacho anasema atakiita Christina Talk Show na kwamba kitakuwa kikijadili masuala mbalimbali ya kijamii bila kubagua kabila au dini kwani lengo ni kuisaidia jamii ya Watanzania.

Mwimbaji huyo ambaye ni mke wa mtu, wamebahatika kupata watoto watatu anasema amesoma hadi kidato cha nne kisha akasomea masuala ya Teknolojia ya Mawasiliano (IT) katika Kituo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UCC), lakini matarajio yake ni kujiunga na Chuo Kikuu kwa ajili ya kupata elimu zaidi.

“Ndoto yangu Mungu akinisaidia nataka mwakani niingine chuo kikuu na nikitoka huko niwe Daktari wa Taaluma. Lengo langu ni kusomea Uongozi wa Biashara, nataka pia kuchukua kozi ya muziki ili kuongeza ujuzi zaidi,” anasema na kuongeza kuwa anataka kuchukua masuala ya uongozi wa biashara kwa sababu hata muziki, ubunifu vyote vinahitaji usimamizi.

Chanzo: Habari Leo

Sunday, April 24, 2011

Tamasha la Pasaka: Hivi Lengo ni Kupagawisha Mashabiki au Kuhubiri Neno ???

Wasanii watamba kupagawisha kesho

Imeandikwa na Mwandishi Wetu
Tarehe: 22nd Aprili 2011 


WASANII watakaotumbuiza kwenye Tamasha la Pasaka wametamba kuwa kesho watatoa burudani ya nguvu kwa mashabiki watakaojitokeza. 



Tamasha la Pasaka litafanyika kesho kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, kisha Jumatatu Uwanja wa Jamhuri Dodoma na Jumanne Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. 


Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama alisema maandalizi yote muhimu yamekamilika na kuwa karibu wasanii wote muhimu tayari wameshafika Dar es Salaam. 


Kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari aliyoitoa Msama, inawakariri wasanii mbalimbali wakizungumzia tamasha hilo, huku wakitamba kwamba mambo yatakuwa mazuri kesho. 

“Nimedhamiria kuwapa mambo mazuri mashabiki wangu, najua watafurahi sana, watakaokuja hawatajuta,” ni kauli ya Rose Muhando. 


Naye msanii Upendo Nkone, amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi na kuwa wana imani kubwa litakuwa tamasha la kufunga mwaka. 


Wasanii wengine wa Tanzania ambao pia wamezungumzia tamasha hilo ni Martha Mwaipaja, Christina Shusho na Boniface Mwaitege, kila mmoja akitamba mashabiki watafurahi. 


Wasanii wa nje ya Tanzania ambao pia wamezungumzia tamasha hilo ni Annastazia Mukabwa, Solomon Mukubwa, Pamera Wanderwa na Geraldine Odour kutoka nchini Kenya. 


Wengine watakaotumbuiza kesho ni Faraja Ntaboba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo anayetamba na kibao cha Hakuna Kama wewe na Ephraem Sekeleti kutoka Zambia.

Chanzo: Habari Leo

~~~~~~~~~

Sunday, April 17, 2011

Mwingira Amtangazia Kifo Babu wa Loliondo


- Adai siku zake za kuishi zinahesabika

Kiongozi mkuu wa huduma ya Efatha, Mtume na Nabii Josephat Mwingira amemtangazia kifo Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwaisapila, maarufu kama Babu wa Loliondo, huku akisema siku za babu huyo kuishi sasa zinahesabika.

Akitoa tangazo hilo mbele ya waumini katika makao makuu ya huduma hiyo Mwenge, jijini Dar es salaam, Jumapili iliyopita, Mwingira alisema babu Mwasapila atakufa kwa kuwa amemtukana Mungu wa Mwingira kwa kuzidi kutamka kuwa tiba anayoitoa imetoka kwa Mungu.

Mwingira ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache tu tangu atangaze rasmi vita dhidi ya Babu Mwasapila. Akitangaza vita  hiyo, Mwingira aliilaani tiba ya Babu huku akisema; “itoweke na iangamie kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti”

Katika tukio la Jumapili iliyopita, mwingira alisoma andiko kutoka Waebrania 1:1-2, kisha akasema Mungu haongei na miti huongea na wanadamu ambao ni watumishi wake. Aliendelea kusema kuwa, babu wa Loliondo amemkasirisha sana kwa kuwa amemtukana Mungu kwa kusema kwamba Mungu ameongea na miti na badala ya watumishi wake.

“Mungu haongei na miti, anaongea na watumishi wake, hata katika kuponya Mungu ameagiza tuweke mikono kwa wagonjwa, Marko 16:15-18 inafafanua hili. Sasa kwa sababu babu wa Loliondo amemtukana Mungu, naye siku zake zinahesabika, kwani Biblia inasema usimwache mchawi kuishi” alisema Mwingira.

Wakati akiendelea na mahubiri yake huku akipita kuombea wenye shida mbalimbali, ghafla alifuatwa na mtumishi mmoja wa kanisa hilo na kumweleza kuwa, ndani ya kanisa hilo amekamatwa msichana ambaye ametumwa kuloga ili kuharibu kazi ya Mungu.

Hata hivyo, Mwingira hakuonesha kushtushwa na taarifa hiyo badala yake aliendelea kuombea watu huku akisema; “mimi sitishwi na wachawi” baadaye wakati akiendelea kuombea watu waliofika eneo ambalo msichana huyo alikuwa ameanguka na kuamuru ainuliwe ili amhoji.

Miongoni mwa maswali aliyoulizwa msichana huyo ni wapi alikotokea na alikuwa ametumwa na nani. Katika majibu yake msichana huy0 alieleza kuwa ametokea Ngorongoro na ametumwa na mtu aliyedai amechoshwa na maombi ya Mwingira yanayokwamisha kazi zake za kichawi. Msichana huyo alitaja jina la aliyemtuma ambaye hatuwezi kuandika jina lake.

Msichana huyo alikutwa na pete yenye picha ya mtu aliyetajwa na msichana huyo kuwa ndiye kamtuma, pamoja na chuma kilichochongwa mfano wa fuvu lililobebwa na ndege pamoja na bangili kubwa ya shaba.

Baadaye Mwingira alimuuliza; “sasa nikufanye nini”? yule msichana akajibu; “naomba unisamehe sitarudia tena ufanya uchawi na sitarudi kule nilikotoka” Mwingira akamuuliza tena; “Unakubali kumpokea Yesu”? yeye akajibu; “ndiyo” Baadaye msichana huyo aliongozwa sala ya toba.

Mwingira ni mmoja wa viongozi wa dini ya kipentekoste ambao walikuwa wa kwanza kabisa kutangaza kuipinga tiba ya Babu wa Loliondo.

Kwa habari zaidi kuhusu babu wa Loliondo, bofya HAPA

Tuesday, April 5, 2011

Miriamu Lukindo Kuzindua Albamu yake Mpya Tarehe 10 Mwezi Huu.


MSANII wa muziki wa injili nchini Miriam Lukindo Mauki anatarajia kuzindua video ya albamu yake ya pili iitwayo "Ni asubuhi". Uzinduzi huo utafanyika Aprili 10 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee,jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari asubuhi hii, Miriam alisema ili kupamba uzinduzi huo wasanii mbalimbali wa muziki wa Injili watasindikiza. Aliwataja wasanii hao kuwa ni pamoja Christina Shusho, Jackson Bent, Martha Mwaipaja, The Voice Band, The Whispers, Makuti Kawe na Marion Shako kutoka Nchini Kenya.

Nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo ni pamoja na Ni asubuhi, Sema na Moyo wanghu, Anasikia, Amefanya, Wewe ni sababu, Mungu yu Mwema, Twende na Yesu na Amen Amen.

Aidha, kiingilio katika uzinduzi huo kimepangwa kuwa ni sh.10,000 kwa viti maalum na 5,000 kwa viti vya kawaida.

 Chanzo: Mtaa kwa Mtaa
*************


Nyongeza


Uzinduzi wa albamu hiyo ulifana sana. Kwa picha zaidi kuhusu uzinduzi huo tembelea HAPA.

Monday, April 4, 2011

ROSE MUHANDO SAFARINI LOLIONDO ???

Malkia wa muziki wa Injili nchini, Rose Muhando, amedai kupanga safari ya kwenda  kijiji cha Samunge, wilayani Loliondo kukutana na Mchungaji, Ambilikile Mwasapile kwa lengo la kunywa dawa ili siku ya Tamasha la Pasaka linalotarajiwa kufanyika mwezi ujao limkute akiwa fiti.

Rose alitoa kauli hiyo hivi karibuni ndani ya  Studio za Zoom Production, zilizopo Magomeni Usalama jijini Dar es Salaam anakorekodia nyimbo zake kumi kwaajili ya albamu yake ya tatu.

Mkali wa Injili ambaye nyimbo zake huonekana mpya kila kukicha alisema kuwa, baada ya kupata taarifa ya tiba za Babu huyo alikuwa na mashaka nazo lakini kadiri siku zinavyokatika ameanza kuziamini kutokana na ushuhuda za watu mbalimbali wanaohudumiwa.

Endapo Rose atatekeleza adhima yake hiyo, atakuwa mwimbaji wa kwanza wa muziki huo kujitangaza kwenda kupata tiba kwa Babu wa Loliondo ambayo imekuwa ikiwagawa watumishi mbalimbali wa Mungu ambao kila mmoja amekuwa akisema lake.

Chanzo: Blogu ya Kabula George

MUKUBWA: MKONO MMOJA HAUNIZUII KUPAGAWISHA MASHABIKI TAMASHA LA PASAKA

 Mukubwa: Mkono mmoja haunizuii kupagawisha mashabiki

Imeandikwa na Mwandishi Wetu
Tarehe: 1 Aprili 2011

KATIKA tamasha la Pasaka mwaka 2010 lililopambwa kwa muziki wa Injili kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, nyoyo za mashabiki zilikongwa na waimbaji kochokocho waliotumbuiza.

Lakini kivutio kikubwa walikuwa ni mwimbaji wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo anayeishi Kenya, Solomon Siaka Mukubwa na Rose Muhando, ambao mara kwa mara kelele za mashabiki zilisikika wakitaka kila mmoja aendelee kuwapa burudani.

Mbali ya Rose Muhando ambaye wimbo wake wa Nibebe uliteuliwa kuwa Wimbo Bora wa Mwaka 2009 kupitia televisheni ya Taifa, TBC1 na Mukubwa, wasanii wengine walioshiriki ni Flora Mbasha na Upendo Nkone.

Waimbaji wengine ni Bahati Bukuku, Jennifer Mgendi, Geraldine Oduor, Enock Jonas, na kundi la muziki wa Injili la Upendo la Kijitonyama, Dar es Salaam. Lakini Mukubwa na Rose ndio waliokuwa kivutio zaidi kutokana na kushangiliwa kwa nguvu.

Mukubwa anasema hamasa aliyoipata mwaka jana ndiyo inampa msukumo zaidi wa kuendelea kukonga nyoyo za mashabiki katika tamasha la mwaka huu.

Tamasha la mwaka huu litafanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Aprili 24 mwaka huu, kisha litarindima kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Aprili 25 na kisha kutibwirika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Aprili 26 mwaka huu ambayo itakuwa Sikukuu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama anasema kwa vile tamasha la mwaka jana lilikuwa la mafanikio makubwa, anaamini hata mwaka huu watavuka malengo ya kukusanya fedha kwa ajili ya watoto yatima, kuwasaidia mitaji ya biashara wajane
wasiojiweza na waathirika wa mabomu yaliyotokea kambi ya JWTZ Gongo la Mboto, Dar es Salaam, Februari 16 mwaka huu.

Wasifu wa Mukubwa ni mlemavu wa mkono mmoja wa kushoto anaodai umekuwa katika hali hiyo kutokana na kudhuriwa kwa uchawi na mama yake wa kambo alipokuwa na umri mdogo.
Anasema akiwa na miaka 12 alipata matatizo hayo kwa kutokea uvimbe wa ajabu na hakuna aliyejua tatizo lilikuwa nini, lakini walibaini kuwa ni mama yake wa kambo ndiye alimroga kutokana na wivu.

Mukubwa anayetamba na wimbo wa 'Mfalme wa Amani', anabainisha kwamba aliugua kwa miaka mitatu na alihaha huku na huko hospitalini hadi kwa waganga wa kienyeji kusaka tiba, lakini hakufanikiwa.

Kwa mantiki hiyo, alifikia uamuzi wa kukatwa mkono kwa vile ulikuwa umeharibika. Mukubwa ametoa albamu mbili ambazo ni Sijaona Rafiki na 'Mungu Mwenye Nguvu'. Mukubwa anasema mama yake huyo wa kambo alikiri kumroga baada ya kuokoka, hivyo amemsamehe.

Anasema mkono huo aliokatwa haumzuii kumuimbia Mungu. Mukubwa anasema alihamia
Kenya kutokana na msaada wa mwimbaji wa nyimbo za Injili, Angela Chibalonza (sasa marehemu), aliyekuwa mshauri wake.

Mukubwa amezaliwa kwenye familia ya watoto tisa, wanaume saba na wanawake wawili, yeye akiwa wa kwanza, ameoa kwa kufunga ndoa na Betty Japhet, Machi mwaka jana. Wengine watakaoshiriki mbali na Mukubwa, wengine watakaoshiriki tamasha la Pasaka mwaka huu ni mwimbaji wa muziki wa Injili kutoka Zambia, Ephraim Sekeleti.

Mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jakaya Kikwete. Kiingilio katika tamasha hilo kitakuwa Sh 4,000 kwa viti vya kawaida, viti vya maalumu (B) Sh 10,000 na viti maalumu (A) Sh 20,000. Tiketi za kategoria hiyo hazitauzwa mlangoni.

Msama anasema tiketi za viti maalumu vya VIP A zitakazokuwa kama meza za familia,
watakaohitaji watalazimika kupiga simu selula 0713 383838, 0786 383838 na 0786 373737 ili kupata tiketi na maelezo kinagaubaga.

Mbali na Sekeleti, wasanii wengine wa nyimbo za Injili watakaopamba tamasha hilo ni Rose Muhando, Upendo Nkone, Bony Mwaitege na wanamuziki kutoka Kenya, Anastazia Mukabwa na Pamela Wanderwa.

Tamasha la Pasaka la mwaka huu litashirikisha waimbaji wa nyimbo za Injili kutoka nchi sita ambazo ni Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini na Zambia.

Pia kutakuwa na kwaya mbili kutoka katika nchi hizo.

Chanzo: Habari Leo

Tuesday, March 22, 2011

ETI, KUTUMIA LUGHA YENYE KUONYESHA USAWA WA KIJINSIA KATIKA BIBLIA (ZA KISASA) NI "KUCHAKACHUA" NENO LA MUNGU?

Kwa tunaoamini kwamba Biblia ni neno la Mungu, ni sawa kweli kuibadilishabadilisha mara kwa mara ili lugha yake iendane na wakati uliopo na mazingira tuliyomo? 

Swali hili limezuka baada ya wafasri wa toleo jipya la mwaka huu la Biblia inayopendwa sana ya New International Version Bible (NIV) kuamua kutumia lugha inayoakisi usawa wa kijinsia. Kwa mfano, badala ya kusema, "If anyone says, 'I love God,' yet hates his brother, he is a liar.", sasa Biblia hiyo inasomeka "If anyone says, "I love God,' yet hates his brother or sister, he is a liar."

Kuna wanaodai kwamba Biblia ni neno la Mungu na kamwe haipaswi kuwa inabadilishwabadilishwa kila mara mikondo au matapo ya mawazo yanapobadilika  katika jamii kwani kwa kufanya hivyo itafikia mahali tutakuwa tunapotosha kabisa maana iliyokusudiwa. Wewe unasemaje kuhusu suala hili?

Kwa habari zaidi kuhusu utata huu wa tafsiri bofya HAPA (Tazama maoni mengi yaliyotolewa hapo). Unaweza pia kusoma kitabu kinachochambua japo hili kwa kina HAPA (pdf - kurasa 357)

Thursday, March 17, 2011

MWAITEGE APANIA TAMASHA LA PASAKA

Mwaitege apania Tamasha la Pasaka
Thursday, 17 March 2011 09:53
Na Mwandishi Wetu, jijini

MWIMBAJI nyota wa muziki wa injili nchini, Bonny Mwaitege, amesema amejipanga vizuri kuhakikisha anafikisha neno la Mungu kwa njia ya muziki wakati wa Tamasha la Pasaka Aprili 24, mwaka huu kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam. Akizungumza na gazeti hili leo asubuhi, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Msama Promotions, Alex Msama, amesema mwimbaji huyo kutoka mkoani Mbeya, alithibitisha kushiriki tamasha hilo na kuahidi kutoa nyimbo mpya.

"Mambo yanazidi kuwa mazuri, sasa tumemaliza mazungumzo na Maitege, amekubali kupanda jukwaani Aprili 24, mwaka huu," amesema.

Msama amewataja waimbaji wengine nyota waliothibitisha kupanda jukwaani wakati wa Tamasha la pasaka ni Rose Muhando, Upendo Nkone, Anastazia Mukabwa na Pamela Wamarwa kutoka Kenya.

Amesema Rose, katika tamasha hilo atatumia nafasi hiyo kuwapa vitu vizuri watu watakaohudhuria tamasha hilo, tayari amekamilisha nyimbo tano mpya zitakazosikika katika tamasha hilo.

Msama amesema kwa upande wa Anastazia, yeye atatumia nafasi hiyo kuwaonesha ubora wa albamu yake ya Vua Kiatu, aliyoimba kwa kushirikiana na Rose Muhando.

Tamasha la Pasaka la mwaka huu litafanyika Aprili 24,  mwaka huu jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda mkoani Dodoma Aprili 25 na Shinyanga Aprili 26."Pamoja na kuwapata nyota hawa watano, bado tunafanya mazungumzo na wengine, tukikamilisha, tutawatangazia," amesema.

Albamu ya Vua Kiatu ina nyimbo nane ambazo ni Vua Kiatu uliobeba jina la albamu hiyo, Ee Mungu, Usiwe Manamba, Nzizilela, Nishike Mkono Bwana, Wanaokudharau na Mfalme.

Kwa mujibu wa Msama, tamasha la Pasaka la mwaka huu, lengo lake kubwa ni kukusanya fedha za kuwasaidia watoto yatima na mitaji ya wanawake wajane.Pia, fedha zitakazopatikana katika tamasha hilo zitatumika kuwasaidia waathirika wa mabomu yaliyotokea katika kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Gongo la Mboto, Dar es Salaam.

Tamasha la Pasaka la mwaka huu litashirikisha waimbaji wa nyimbo za injili kutoka nchi sita ambazo ni Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Afrika Kusini na Zambia.

Chanzo: Dar Leo

Monday, March 14, 2011

KIKWETE MGENI RASMI TAMASHA LA PASAKA


Kikwete mgeni rasmi Tamasha la Pasaka

Na Mwandishi Wetu; Tarehe: 14th March 2011

RAIS wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete atakuwa mgeni rasmi wa Tamasha la Pasaka litakalofanyika siku ya sikukuu ya Pasaka, Aprili 24 mwaka huu katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha la Pasaka ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Msama Promotions waandaaji wa tamasha hilo, Alex Msama ilieleza kuwa Rais tayari amethibitisha kuhudhuria.

Alisema Rais Kikwete amekubali kujumuika na wadau mbalimbali katika tamasha hilo la aina yake na kwamba litakuwa bora kuliko matamasha mengine yaliyopita.

Alimshukuru Rais Kikwete kwa kukubali mwaliko wao na kuongeza kuwa hiyo ni furaja kwa waandaaji pamoja na Wakristo wote kwa vile siku hiyo ni sikukuu ya Pasaka.

Kwa mujibu wa Msama kiasi cha fedha kitakachopatikana kwenye tamasha hilo kitatumika kuwasaidia waathirika wa mabomu ya Gongo la Mboto, Dar es Salaam.

Hata hivyo Msama alisema kwamba lengo la awali la kuwasomesha yatima na kuwasaidia mitaji ya biashara wanawake wajane bado lipo pale pale.

“Pamoja kwamba tutawasaidia waathirika wa mabomu pia, lile lengo letu kubwa la tamasha hili kuwasaidia kuwasomesha yatima na wajane lipo pale pale,” alisema.

Chanzo: Habari Leo

Sunday, September 26, 2010

BISHOP EDDIE LONG KATIKA KASHFA NZITO YA MAPENZI YA KISHOGA

  • Mtumishi wa Mungu mwenye uwezo mkubwa wa kuhubiri Neno Bishop Eddie Long (na mpinzani mkubwa wa mahusiano ya kishoga) mambo yamembumburukia (kama wenzake hawa) baada ya kushushiwa tuhuma nzito na wavulana wanne ambao walikuwa waumini wa kanisa lake. Wavulana hawa tayari wameshafungua kesi mahakamani na mwingine wa tano anategemea kufanya hivyo hivi karibuni.
  • Wavulana hawa wanadai kwamba Bishop alikuwa akiwalaghai kwa pesa, magari, vito vya thamani na safari za ndani na nje ya Marekani huku akijifanya kuwa kama "baba" kwao na baadaye kutumia nafasi hiyo kuanzisha uhusiano wa kingono. 
  • Habari hizi zipo kila mahali hapa Marekani na sasa kuna picha ambazo zinadaiwa kwamba Bishop alikuwa akiwatumia vijana hawa na "text messages" ambazo alikuwa akiwaomba pia wamtumie picha zao. Na kwa wanaopenda kuhukumu, tayari wameanza kupaza sauti wakidai ni lazima ajiuzulu wadhifa wake kama Mchungaji Mkuu wa kanisa kubwa la New Birth Missionary Baptist Church lenye waumini wapatao 25,000 wakiwemo watu mashuhuri mbalimbali.
  • Watu wengi wanatumaini kwamba tuhuma hizi ni za uwongo na pengine wavulana hawa wanataka pesa. Lakini kwa vyo vyote vile hili si jambo jema. Mungu Atusaidie sote na kutupa rehema zake ambazo bila kwazo kamwe hatuwezi kuokolewa! Tukumbuke kwamba hakuna aliye mkamilifu.

Thursday, September 2, 2010

BREAKING NEWS: UPENDO NKONE KUFUNGA NDOA OKTOBA 17, 2010

  • Kama ambavyo tuliwahi kuandika hapa juu ya uchumba wa Upendo Nkone - mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za Injili nchini Tanzania, harusi yake sasa imewadia. Mtumishi huyu wa Bwana anatarajia kufunga ndoa na Mchungaji John Mbeyela oktoba 17 mwaka huu.
  • Habari zilizopatikana kupitia gazeti la Majira zinaeleza kwamba Upendo Nkone ataagwa nyumbani kwao Kigoma Oktoba 11 na ndoa yake na mchungaji huyo ambaye naye ni mjane mwenye watoto watatu itafungwa katika kanisa la Naioth maarufu Kwa Mwasota lililopo Mabibo Makuburini jijini Dar es salaam. 
  • Mwimbaji huyo mashuhuri alianza kuimba miaka mitano iliyopita na mpaka sasa amefanikiwa kutoa albamu tatu ambazo ni Mungu Baba, Hapa Nilipo na Zipo faida. 
  • Mtumishi, tunakutakia kila la heri katika ndoa yako

Saturday, August 28, 2010

FLORA MBASHA KATIKA BURUDANI NDANI YA MKUTANO MKUU WA CCM, KIZOTA DODOMA

  • Mwanamuziki maarufu wa nyimbo za injili Flora Mbasha na kundi lake zima waliinua mashabiki wengi wa nyimbo za injili na wimbo wao uliokuwa na speed ya kasi na uliowasisimua wengi. Wimbo huo ulisifu uongozi wa Mwenyekiti wa CCM ukisihi kuongeza ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi kuleta maendeleo Tanzania.
  • Baadhi ya "wadau" wa nyimbo za injili wameshaonyesha kukerwa na tabia hii ya waimbaji wa injili kutumbuiza katika majukwaa ya kisiasa. Msomaji wa blogu hii, wewe una maoni gani kuhusu suala hili?
  • Habari hii inapatikana hapa.

Sunday, August 22, 2010

MSAMA AKEMEA WAIMBA INJILI KUTUMBUIZA MAJUKWAA YA SIASA

ALEX MSAMA

MKURUGENZI mashuhuri wa kampuni ya Msama Promotion Alex Msama amekemea mtindo ulioibuka hivi karibuni wa wanamuziki wa Injili kujitokeza kutumbuiza katika majukwaa ya kisiasa.

Msama amesema wao ni wainjilisti na si wanasiasa hivyo waache kutumika katika majukwaa ya kisaasa sambamba na kushiriki katika kampeni. Alisema kufanya hivyo ni kumtumikia shetani kwani hawana tofauti na waimbaji wa bongo fleva. 

Chanzo: Mamapipiro.

Monday, July 19, 2010

UJUMBE MZURI KUTOKA MWANZA

  • Niliipiga picha hii mwezi wa sita mwaka huu pale Mtaa wa Uhuru jijini Mwanza. Ujumbe mzuri!

Friday, July 16, 2010

KAKOBE ALIPULIWA - NA HERRIETH BENNY WA GAZETI LA MTANZANIA


MUUMINI wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), la Askofu Mkuu Zachary Kakobe, ameibuka na kutoa siri nzito kuhusu Kanisa hilo.
 
Mtoa siri huyo ni Mchungaji Monicah Mtasingwa, ambaye pamoja na mambo mengine, ameeleza ubabe, ukiukwaji wa haki za binadamu na adha za maisha zinazowafanya wachungaji na waumini wa Kanisa waishi kwa shida.
 
Mtasingwa alitoa siri za Askofu Mkuu Kakobe jana alipozungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) jijini Dar es Salaam.

Alisema miongoni mwa adha walizoonja kwa kuwapo kwao kwa Kakobe ni kuuza mali zao zote kwa ajili ya kuanzisha tawi la Kanisa hilo, lakini wameishia kupokwa kila kitu.

Alisema Askofu Mkuu Kakobe anatumia vitisho kuwakandamiza wachungaji wake wasijiendeleze kielimu huku akiwambia kuwa yeyote atakayekiuka sheria zake atakufa.

Kitu kingine ni kwamba wachungaji na waumini wanazuiwa kushirikiana na watu wa madhehebu mengine kwa madai kwamba ni wazinzi na makahaba.

Mtasingwa alisimulia jinsi yeye na mumewe walivyoweza kuingia katika Kanisa hilo, na kufikia hatua ya kwenda kuanzisha tawi Nzega.

“Wakati huo mume wangu alikuwa mfanyakazi wa benki, mimi nilikuwa nimemaliza kidato cha sita Msalato mkoani Dodoma, tulipofika huko tulianza kuishi maisha ya kimasikini, hata hivyo tuliweza kujenga kanisa na makazi yetu ambayo hivi sasa yamechukuliwa.

“Niliamua kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa siri  ambako nilisoma sayansi ya jamii ili niwe mchungaji mwenye uelewa, lakini Askofu Kakobe aliposikia alisema mimi ni fisadi, akanitenga na mume wangu wa ndoa.

“Hata hivyo, mume wangu baadaye alijutia kosa, nilirudi Nzega, Askofu Kakobe aliposikia hivyo alimfukuza kazi na kutunyang’anya kila tulichokuwa nacho,” alisema Mtasingwa.

Alisema Askofu Mkuu Kakobe hajawahi kuwapa Katiba waumini waione, hali iliyomfanya yeye Mtasingwa aitafute kwa udi na uvumba.

Alisema alifanikiwa kuipata na kubaini kuwa wanatakiwa kusoma ili kupambana na mafisadi.

“Ninamuomba Askofu Kakobe aache kutoa vitisho juu ya familia yetu, usalama wetu wa maisha kule Nzega ni mdogo kwani hata polisi nao hawajalichukulia uzito pamoja na kutoa taarifa,” alisema.

Aliwaonya Wakristo kuacha kutangatanga makanisani kwa kudhani kuwa wanamtafuta Mungu, kwani wanaweza kukutana na mateso kama yaliyowapata.

“Wakristo simamieni wokovu, ni wewe siyo kanisa, simama ulipo usiondoke, Kakobe hata vyeti vya ndoa hatoi kutokana na ukandamizaji alionao, amebeba madaraka yote yeye mwenyewe, Kanisa limekuwa ni asasi ya kujinufaisha mwenyewe, anapoulizwa kuhusu jambo anasema hakuna kuhoji hoji,” alisema.

Hii si mara ya kwanza kwa waliokuwa waumini wa Aksofu Kakobe kujitokeza hadharani kuanika udhaifu na dhuluma ndani ya Kanisa hilo.

Juhudi za kumpata Askofu Mkuu Kakobe kuzungumzia tuhuma hizi mpya zilishindikana. Muda wote simu yake ya mkononi ilipopigwa haikupokewa.

*******************
Habari hii inapatikana hapa.