Audio ya Sinema ya Yesu Katika Kisukuma
  
Audio ya Sinema ya Yesu Katika Kiswahili

Monday, April 4, 2011

MUKUBWA: MKONO MMOJA HAUNIZUII KUPAGAWISHA MASHABIKI TAMASHA LA PASAKA

 Mukubwa: Mkono mmoja haunizuii kupagawisha mashabiki

Imeandikwa na Mwandishi Wetu
Tarehe: 1 Aprili 2011

KATIKA tamasha la Pasaka mwaka 2010 lililopambwa kwa muziki wa Injili kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, nyoyo za mashabiki zilikongwa na waimbaji kochokocho waliotumbuiza.

Lakini kivutio kikubwa walikuwa ni mwimbaji wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo anayeishi Kenya, Solomon Siaka Mukubwa na Rose Muhando, ambao mara kwa mara kelele za mashabiki zilisikika wakitaka kila mmoja aendelee kuwapa burudani.

Mbali ya Rose Muhando ambaye wimbo wake wa Nibebe uliteuliwa kuwa Wimbo Bora wa Mwaka 2009 kupitia televisheni ya Taifa, TBC1 na Mukubwa, wasanii wengine walioshiriki ni Flora Mbasha na Upendo Nkone.

Waimbaji wengine ni Bahati Bukuku, Jennifer Mgendi, Geraldine Oduor, Enock Jonas, na kundi la muziki wa Injili la Upendo la Kijitonyama, Dar es Salaam. Lakini Mukubwa na Rose ndio waliokuwa kivutio zaidi kutokana na kushangiliwa kwa nguvu.

Mukubwa anasema hamasa aliyoipata mwaka jana ndiyo inampa msukumo zaidi wa kuendelea kukonga nyoyo za mashabiki katika tamasha la mwaka huu.

Tamasha la mwaka huu litafanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Aprili 24 mwaka huu, kisha litarindima kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Aprili 25 na kisha kutibwirika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Aprili 26 mwaka huu ambayo itakuwa Sikukuu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama anasema kwa vile tamasha la mwaka jana lilikuwa la mafanikio makubwa, anaamini hata mwaka huu watavuka malengo ya kukusanya fedha kwa ajili ya watoto yatima, kuwasaidia mitaji ya biashara wajane
wasiojiweza na waathirika wa mabomu yaliyotokea kambi ya JWTZ Gongo la Mboto, Dar es Salaam, Februari 16 mwaka huu.

Wasifu wa Mukubwa ni mlemavu wa mkono mmoja wa kushoto anaodai umekuwa katika hali hiyo kutokana na kudhuriwa kwa uchawi na mama yake wa kambo alipokuwa na umri mdogo.
Anasema akiwa na miaka 12 alipata matatizo hayo kwa kutokea uvimbe wa ajabu na hakuna aliyejua tatizo lilikuwa nini, lakini walibaini kuwa ni mama yake wa kambo ndiye alimroga kutokana na wivu.

Mukubwa anayetamba na wimbo wa 'Mfalme wa Amani', anabainisha kwamba aliugua kwa miaka mitatu na alihaha huku na huko hospitalini hadi kwa waganga wa kienyeji kusaka tiba, lakini hakufanikiwa.

Kwa mantiki hiyo, alifikia uamuzi wa kukatwa mkono kwa vile ulikuwa umeharibika. Mukubwa ametoa albamu mbili ambazo ni Sijaona Rafiki na 'Mungu Mwenye Nguvu'. Mukubwa anasema mama yake huyo wa kambo alikiri kumroga baada ya kuokoka, hivyo amemsamehe.

Anasema mkono huo aliokatwa haumzuii kumuimbia Mungu. Mukubwa anasema alihamia
Kenya kutokana na msaada wa mwimbaji wa nyimbo za Injili, Angela Chibalonza (sasa marehemu), aliyekuwa mshauri wake.

Mukubwa amezaliwa kwenye familia ya watoto tisa, wanaume saba na wanawake wawili, yeye akiwa wa kwanza, ameoa kwa kufunga ndoa na Betty Japhet, Machi mwaka jana. Wengine watakaoshiriki mbali na Mukubwa, wengine watakaoshiriki tamasha la Pasaka mwaka huu ni mwimbaji wa muziki wa Injili kutoka Zambia, Ephraim Sekeleti.

Mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jakaya Kikwete. Kiingilio katika tamasha hilo kitakuwa Sh 4,000 kwa viti vya kawaida, viti vya maalumu (B) Sh 10,000 na viti maalumu (A) Sh 20,000. Tiketi za kategoria hiyo hazitauzwa mlangoni.

Msama anasema tiketi za viti maalumu vya VIP A zitakazokuwa kama meza za familia,
watakaohitaji watalazimika kupiga simu selula 0713 383838, 0786 383838 na 0786 373737 ili kupata tiketi na maelezo kinagaubaga.

Mbali na Sekeleti, wasanii wengine wa nyimbo za Injili watakaopamba tamasha hilo ni Rose Muhando, Upendo Nkone, Bony Mwaitege na wanamuziki kutoka Kenya, Anastazia Mukabwa na Pamela Wanderwa.

Tamasha la Pasaka la mwaka huu litashirikisha waimbaji wa nyimbo za Injili kutoka nchi sita ambazo ni Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini na Zambia.

Pia kutakuwa na kwaya mbili kutoka katika nchi hizo.

Chanzo: Habari Leo

No comments: