MAHUBIRI YA MZEE WA UPAKO NA MTUME/NABII JOSEPHAT MWINGIRA

Mahubiri ya Mzee wa Upako

Mahubiri ya Mtume na Nabii Josephat Mwingira

Tuesday, September 13, 2011

Christina Shusho: Gwiji wa Injili Anayepasua Anga za Kimataifa

CHRISTINA SHUSHO: Gwiji wa Injili Anayepasua Anga za Kimataifa
Na Angela Semaya; Tarehe 7 Septemba 2011 

“UNIKUMBUKE Babaa unapowazuru wengine naomba unikumbuke, usinipite Yesu unapowazuru wengine naomba unikumbuke, unikumbuke babaa unapowazuru wengine naomba unikumbuke…”

Haya ni baadhi ya maneno yaliyomo katika moja ya nyimbo zinazomtambulisha vyema Mwimbaji wa Nyimbo za Injili, Christina Shusho.

Shusho amefanikiwa kujijengea sifa kwa mashabiki wa nyimbo za Injili ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kutokana na nyimbo zake kubeba ujumbe mzito kwa jamii, lakini ukiwa katika msingi wa neno la Mungu ambalo analiamini.

Umahiri wake katika kuimba nyimbo za Injili umemuwezesha Shusho kutambulika vyema na kujinyakulia Tuzo mbalimbali ikiwemo Tuzo aliyopata wiki chache zilizopita huko Nairobi, Kenya.

Shusho alikuwa kati ya wasanii wa Tanzania waliopata Tuzo za Muziki za Afrika Mashariki na Kati (EMAS) zilizofanyika Agosti 20, mwaka huu na kushirikisha wasanii mbalimbali wa kutoka nchi nane za Afrika Mashariki na Kati.

Mwimbaji huyo aliibuka na Tuzo ya Msanii Bora wa Kike wa Nyimbo za Injili akiingia na wimbo wake Unikumbe na kumshinda mwimbaji mwenzake kutoka Tanzania Upendo Nkone aliyeingia na wimbo wake Haleluya Usifiwe, Alice Kamande kutoka Kenya na wimbo wake Upendo na Gaby kutoka Rwanda na wimbo wake Amahoro.

Wasanii wengine wa Tanzania walioshinda Tuzo hizo ni Bendi ya Muziki wa Dansi ya Msondo, Ambwene Yesaya `AY’ na Khamis Mwinjuma `Mwana FA’. Kutokana na ushindi huo, HABARILEO Jumapili lilipata fursa ya kukutana na kuzungumza na Shusho kuhusiana na ushindi huo, kazi yake, maisha yake na mafanikio aliyopata kutokana na uimbaji wake wa muziki wa Injili.

Akizungumzia Tuzo hiyo, Shusho ambaye ni mama wa watoto watatu anasema ni heshima kubwa kwa Mungu na kwake hasa kwa kuwa alishindanishwa na wanamuziki wenye vipaji vikubwa vya uimbaji wa nyimbo za Injili akiwemo mwimbaji mwenyeji Alice.

“Kidogo nilipata hisia za woga iwapo nitashinda hasa kutokana na ushiriki wa Alice ambaye ni mwimbaji mzuri wa nyimbo za Injili, lakini pia shindano lilifanyika nchini kwao hivyo mashabiki wake nilihisi kuwa ni wengi zaidi, lakini Mungu ni mwema nikapata mimi hiyo Tuzo hivyo nina kila sababu ya kumshukuru Mungu,” anasema.

Shusho anasema ushindi huo umemfanya ajisikie kumheshimu na kumnyenyekea zaidi Mungu kwa kumpeleka kila hatua, lakini pia anaona fahari kuwa watu ndani na nje ya mipaka ya Tanzania wanatambua kipaji chake na kazi aliyopewa.

“Naona ushindi huu mbali na kumheshimu Mungu zaidi, lakini pia naona nimepewa jukumu zaidi kwa maana kukitumia kipaji changu nilichopewa kwa kuimba zaidi ya hapa na kufikisha ujumbe kwa jamii kupitia uimbaji wa Injili,” anasema.

Nini msingi au chanzo cha uimbaji wake? Shusho anasema msingi wake umeanzia nyumbani kwa kile alichoeleza kuzaliwa katika familia ya Kikristo ambayo ilipenda kuomba na kusali. “Mimi nimezaliwa katika familia ya kikristo, kwa hiyo Jumapili nilikuwa nikihudhuria Shule ya Jumapili (Sunday School) ambapo watoto tulikuwa tukifundishwa dini, na huko ndipo nilianza kuimba,” anasema.

Anasema alipokuwa akiendelea kukua alijiona kuwa na wito na akaona ajaribu kuimba mwenyewe na kugundua ana kipaji na wito wa kuimba nyimbo za Injili, hivyo alianza kutunga nyimbo zake. “Mwaka 2003/2004 niliamua kuingia Studio.

Baada ya kupata msukumo hasa 2004 nilitengeneza muziki na kuingia studio…unajua nilipoamua tu nikaanza kutunga nyimbo zangu, kwa hiyo niliingia studio na nyimbo zangu mwenyewe,” anasema. Shusho anasema msingi mkubwa wa nyimbo zake ni neno la Mungu.

”Hata kama nitatoa wimbo kwa ajili ya jamii, lakini lazima msingi wake uanze na neno la Mungu.” Kwa mujibu wa mwimbaji huyo, mtindo wa nyimbo wake ni kusifu na kuabudu na kwamba hatungi wimbo kwa msingi wa kumjibu ama kumshambulia mtu zaidi ya kumsifu Mungu kwa ukuu wake.

“Unajua kuna wengine wanaimba nyimbo za Injili, lakini ukiusikiliza uko katika hali ya ama kumjibu mtu au kumshambulia mtu baada ya kuapa jambo fulani. Mimi ni tofauti naimba kumsifu na kumuabudu Mungu,” anasema.

Hadi sasa Shusho ameshatoa Albamu nne ambazo ni Kitu Gani yenye nyimbo nane iliyotoka mwaka 2004/2005, Unikumbuke yenye nyimbo nane iliyotoka mwaka 2007/2008, Nipe Macho yenye nyimbo 10 na Kwa Kanisa la Kristo yenye nyimbo nane ambazo amezitoa pamoja mwaka 2010/2011.

Kwa mujibu wa Shusho, albamu ya Unikumbuke ambayo alizindua rasmi Novemba 30, 2008 ndiyo iliyomtambulisha vyema kwa mashabiki wa muziki wa Injili na hadi sasa ameendelea kufanya vizuri hadi sasa.

Akizungumzia kukua kwa muziki huo anasema muziki wa Injili umekuwa, kwa kile alichoeleza kuwa zamani kwaya ndio zilikuwa zikijulikana lakini tofauti na sasa nyimbo za Injili zimepenya na unakuta zikitambulika katika matamasha na mashindano makubwa ya nyimbo za Injili.

Shusho anasema kuimba kwake nyimbo za Injili kumemuwezesha kupata faida mbalimbali, lakini kwanza jamii kumtambua na kukifahamu kipaji alichonacho, pili kazi zake kutambulika na kukubalika, tatu anajiona kutumika vizuri na kwamba anaamini Mungu anaona anavyofanya vyema kazi yake na nne imemuwezesha kufahamika ndani na nje. “Mungu amenipa maono na mambo ya mbeleni.

Kwa kweli Mungu amekuwa akinibariki kwa njia moja au nyingine,” anasema. Kutokana na uimbaji wake wa nyimbo za Injili Shusho anasema ameweza kushiriki matamasha ya ndani, lakini pia katika nchi za nje ikiwemo Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uingereza.

Mbali na Tuzo ya EMAS ambayo ameipata wiki chache zilizopita lakini pia anasema ameshawahi kupata Tuzo nyingine ikiwemo Tuzo ya Meya Cup iliyotolewa nchini Kenya, Tuzo za Muziki wa Injili (Gospel Music Awards) iliyotolewa hapa nchini ambapo aliibuka mshindi wa Msanii Bora wa Muziki wa Injili na Tuzo ya Kenya Groove Music Awards ambapo aliibuka na Tuzo ya Msanii Bora wa Nje.

Akizungumzia mtindo wa muziki wa Injili hivi sasa anasema, “kila mtu amepewa staili yake ya uimbaji…lakini tunapaswa kukumbuka kila watu wana utamaduni wao kwa hiyo ni vyema tukaimba kuzingatia mazingira yetu. Mungu angefurahi zaidi kama Watanzania tutaimba kwa kuzingatia utamaduni wetu…sidhani kama Mungu asingependa tuimbe kama Wachina, au Wazungu na kadhalika, Mungu atajali tukiimba kwa namna na kipawa alichotupa.”

Anawashukuru mashabiki wake kwa kile anachosema wamemsaidia kwa ushauri wa aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumpa mapendekezo na kwamba wamemshauri abakie na staili yake ya kuimba kwa taratibu.

“Kama nilivyosema nyimbo zangu ziko kwa mtindo wa kusifu na kuabudu ndio maana naimba taratibu na hivyo ni rahisi mtu kusikiliza nyimbo zangu hata akiwa anasikiliza katika redio wakati anaendesha gari njiani au amerudi nyumbani anataka kutulia lakini akisikiliza nyimbo za Injili…mimi najiamini na naamini staili yangu ni njema zaidi na ndio nadhani naimudu,” anasema na kuongeza lengo lake ni kuliimbia kanisa ambalo litaendelea kuwepo milele.

Mbali na kuwa mwimbaji wa nyimbo za Injili, Shusho anasema anapenda kupendeza na kuonekana maridadi na ndio maana pia anajishughulisha na masuala ya ubunifu wa mavazi na pia ananunua bidhaa au vitu kutoka nje.

Lakini pia Shusho ni mtangazaji wa kituo cha televisheni SIBUKA na akiendesha kipindi kinachojulikana kama Gospel Hits.

Hata hivyo anasema lengo lake ni kuanzisha kipindi chake cha televisheni ambacho anasema atakiita Christina Talk Show na kwamba kitakuwa kikijadili masuala mbalimbali ya kijamii bila kubagua kabila au dini kwani lengo ni kuisaidia jamii ya Watanzania.

Mwimbaji huyo ambaye ni mke wa mtu, wamebahatika kupata watoto watatu anasema amesoma hadi kidato cha nne kisha akasomea masuala ya Teknolojia ya Mawasiliano (IT) katika Kituo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UCC), lakini matarajio yake ni kujiunga na Chuo Kikuu kwa ajili ya kupata elimu zaidi.

“Ndoto yangu Mungu akinisaidia nataka mwakani niingine chuo kikuu na nikitoka huko niwe Daktari wa Taaluma. Lengo langu ni kusomea Uongozi wa Biashara, nataka pia kuchukua kozi ya muziki ili kuongeza ujuzi zaidi,” anasema na kuongeza kuwa anataka kuchukua masuala ya uongozi wa biashara kwa sababu hata muziki, ubunifu vyote vinahitaji usimamizi.

Chanzo: Habari Leo

No comments: