Audio ya Sinema ya Yesu Katika Kisukuma
  
Audio ya Sinema ya Yesu Katika Kiswahili

Friday, July 16, 2010

KAKOBE ALIPULIWA - NA HERRIETH BENNY WA GAZETI LA MTANZANIA


MUUMINI wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), la Askofu Mkuu Zachary Kakobe, ameibuka na kutoa siri nzito kuhusu Kanisa hilo.
 
Mtoa siri huyo ni Mchungaji Monicah Mtasingwa, ambaye pamoja na mambo mengine, ameeleza ubabe, ukiukwaji wa haki za binadamu na adha za maisha zinazowafanya wachungaji na waumini wa Kanisa waishi kwa shida.
 
Mtasingwa alitoa siri za Askofu Mkuu Kakobe jana alipozungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) jijini Dar es Salaam.

Alisema miongoni mwa adha walizoonja kwa kuwapo kwao kwa Kakobe ni kuuza mali zao zote kwa ajili ya kuanzisha tawi la Kanisa hilo, lakini wameishia kupokwa kila kitu.

Alisema Askofu Mkuu Kakobe anatumia vitisho kuwakandamiza wachungaji wake wasijiendeleze kielimu huku akiwambia kuwa yeyote atakayekiuka sheria zake atakufa.

Kitu kingine ni kwamba wachungaji na waumini wanazuiwa kushirikiana na watu wa madhehebu mengine kwa madai kwamba ni wazinzi na makahaba.

Mtasingwa alisimulia jinsi yeye na mumewe walivyoweza kuingia katika Kanisa hilo, na kufikia hatua ya kwenda kuanzisha tawi Nzega.

“Wakati huo mume wangu alikuwa mfanyakazi wa benki, mimi nilikuwa nimemaliza kidato cha sita Msalato mkoani Dodoma, tulipofika huko tulianza kuishi maisha ya kimasikini, hata hivyo tuliweza kujenga kanisa na makazi yetu ambayo hivi sasa yamechukuliwa.

“Niliamua kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa siri  ambako nilisoma sayansi ya jamii ili niwe mchungaji mwenye uelewa, lakini Askofu Kakobe aliposikia alisema mimi ni fisadi, akanitenga na mume wangu wa ndoa.

“Hata hivyo, mume wangu baadaye alijutia kosa, nilirudi Nzega, Askofu Kakobe aliposikia hivyo alimfukuza kazi na kutunyang’anya kila tulichokuwa nacho,” alisema Mtasingwa.

Alisema Askofu Mkuu Kakobe hajawahi kuwapa Katiba waumini waione, hali iliyomfanya yeye Mtasingwa aitafute kwa udi na uvumba.

Alisema alifanikiwa kuipata na kubaini kuwa wanatakiwa kusoma ili kupambana na mafisadi.

“Ninamuomba Askofu Kakobe aache kutoa vitisho juu ya familia yetu, usalama wetu wa maisha kule Nzega ni mdogo kwani hata polisi nao hawajalichukulia uzito pamoja na kutoa taarifa,” alisema.

Aliwaonya Wakristo kuacha kutangatanga makanisani kwa kudhani kuwa wanamtafuta Mungu, kwani wanaweza kukutana na mateso kama yaliyowapata.

“Wakristo simamieni wokovu, ni wewe siyo kanisa, simama ulipo usiondoke, Kakobe hata vyeti vya ndoa hatoi kutokana na ukandamizaji alionao, amebeba madaraka yote yeye mwenyewe, Kanisa limekuwa ni asasi ya kujinufaisha mwenyewe, anapoulizwa kuhusu jambo anasema hakuna kuhoji hoji,” alisema.

Hii si mara ya kwanza kwa waliokuwa waumini wa Aksofu Kakobe kujitokeza hadharani kuanika udhaifu na dhuluma ndani ya Kanisa hilo.

Juhudi za kumpata Askofu Mkuu Kakobe kuzungumzia tuhuma hizi mpya zilishindikana. Muda wote simu yake ya mkononi ilipopigwa haikupokewa.

*******************
Habari hii inapatikana hapa.

4 comments:

Anonymous said...

Ninamsikitikia sana Monicah kwa kuthubutu kutunga uongo dhidi ya mtumishi wa Mungu. Kwanza kabisa, Monicah hajawahi kuwa mchungaji wa fgbf, yeye alikuwa mama mchungaji. Kusema kuwa Askofu Kakobe anawanyima watu vyeti vya ndoa ni uongo mwingine, mbona mimi na mke wangu tulipewa. Ushauri wa bure kwa Monicah na wengine wenye tabia kama hiyo "Kazi uliyoitiwa na Mungu na wewe uliipokea kwa hiari yako mwenyewe ikikushinda acha kimya kimya, usitafute visingizio. Uliacha vyote kwa hiari yako mwenyewe ili uende ukamtumikie Mungu, iweje leo unalalamika? Humung'unikii mwanadamu bali Mungu. Kumbuka unajiletea laana wewe mwenyewe. Ni wangapi wailodiriki kushindana na huyu mtumishi na leo hawajafika popote pale"

Anonymous said...

Hizi imani zilizoletwa na wazungu zinatutesa sana waafrika,kuhamahama makanisa kila leo, kuna watu Yesu atawakuta bado wanahamahama na hawajajiandaa kiroho. ndugu zangu wokovu upo kwa Yesu Kristo na wala sio makanisani.

Firstcollina said...

Pole dada Monicah!
Nijuavyo mimi, kila mtu ana haki ya kuzungumza. Hii si mara ya kwanza kusikia mabo kama haya, cha ajabu ni kwamba watu wamekuwa mstari wa mbele kuwalaumu wenzao kwa kusema kile walichokiona.
Nadhani sio siri lazima tukubali kukosolewa na hata wakati mwingine kukosoa. Jambo la uungwana hapa ni kwamba mtu kujisafisha na kubadili njia zake.
Askofu kakobe lazima afike sehemu ajitazame kama biblia inavyosema.....Adhaniaye amesimama aangalie asiangukiwe na mti....!

Anonymous said...

EV. MGENI,T. SEOUL KOREA.
Watanzania nani kawaroga muwasimange watumishi wa mungu aliye hai? Inawezekana kwenu wakawa na makosa lakini ninyi hamumwogopi mungu aliyewapaka mafuta au mnafikiri wokovu ni siasa kila mtu anakosoa? jifunzeni kwa miriamu na haruni HES 12:1-9. Kama mkiona neno nawashauri muwaombee watumishi wa Mungu vinginevyo mnajitafutia laana.