Audio ya Sinema ya Yesu Katika Kisukuma
  
Audio ya Sinema ya Yesu Katika Kiswahili

Sunday, April 17, 2011

Mwingira Amtangazia Kifo Babu wa Loliondo


- Adai siku zake za kuishi zinahesabika

Kiongozi mkuu wa huduma ya Efatha, Mtume na Nabii Josephat Mwingira amemtangazia kifo Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwaisapila, maarufu kama Babu wa Loliondo, huku akisema siku za babu huyo kuishi sasa zinahesabika.

Akitoa tangazo hilo mbele ya waumini katika makao makuu ya huduma hiyo Mwenge, jijini Dar es salaam, Jumapili iliyopita, Mwingira alisema babu Mwasapila atakufa kwa kuwa amemtukana Mungu wa Mwingira kwa kuzidi kutamka kuwa tiba anayoitoa imetoka kwa Mungu.

Mwingira ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache tu tangu atangaze rasmi vita dhidi ya Babu Mwasapila. Akitangaza vita  hiyo, Mwingira aliilaani tiba ya Babu huku akisema; “itoweke na iangamie kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti”

Katika tukio la Jumapili iliyopita, mwingira alisoma andiko kutoka Waebrania 1:1-2, kisha akasema Mungu haongei na miti huongea na wanadamu ambao ni watumishi wake. Aliendelea kusema kuwa, babu wa Loliondo amemkasirisha sana kwa kuwa amemtukana Mungu kwa kusema kwamba Mungu ameongea na miti na badala ya watumishi wake.

“Mungu haongei na miti, anaongea na watumishi wake, hata katika kuponya Mungu ameagiza tuweke mikono kwa wagonjwa, Marko 16:15-18 inafafanua hili. Sasa kwa sababu babu wa Loliondo amemtukana Mungu, naye siku zake zinahesabika, kwani Biblia inasema usimwache mchawi kuishi” alisema Mwingira.

Wakati akiendelea na mahubiri yake huku akipita kuombea wenye shida mbalimbali, ghafla alifuatwa na mtumishi mmoja wa kanisa hilo na kumweleza kuwa, ndani ya kanisa hilo amekamatwa msichana ambaye ametumwa kuloga ili kuharibu kazi ya Mungu.

Hata hivyo, Mwingira hakuonesha kushtushwa na taarifa hiyo badala yake aliendelea kuombea watu huku akisema; “mimi sitishwi na wachawi” baadaye wakati akiendelea kuombea watu waliofika eneo ambalo msichana huyo alikuwa ameanguka na kuamuru ainuliwe ili amhoji.

Miongoni mwa maswali aliyoulizwa msichana huyo ni wapi alikotokea na alikuwa ametumwa na nani. Katika majibu yake msichana huy0 alieleza kuwa ametokea Ngorongoro na ametumwa na mtu aliyedai amechoshwa na maombi ya Mwingira yanayokwamisha kazi zake za kichawi. Msichana huyo alitaja jina la aliyemtuma ambaye hatuwezi kuandika jina lake.

Msichana huyo alikutwa na pete yenye picha ya mtu aliyetajwa na msichana huyo kuwa ndiye kamtuma, pamoja na chuma kilichochongwa mfano wa fuvu lililobebwa na ndege pamoja na bangili kubwa ya shaba.

Baadaye Mwingira alimuuliza; “sasa nikufanye nini”? yule msichana akajibu; “naomba unisamehe sitarudia tena ufanya uchawi na sitarudi kule nilikotoka” Mwingira akamuuliza tena; “Unakubali kumpokea Yesu”? yeye akajibu; “ndiyo” Baadaye msichana huyo aliongozwa sala ya toba.

Mwingira ni mmoja wa viongozi wa dini ya kipentekoste ambao walikuwa wa kwanza kabisa kutangaza kuipinga tiba ya Babu wa Loliondo.

Kwa habari zaidi kuhusu babu wa Loliondo, bofya HAPA

3 comments:

Anonymous said...

Shetani na shetani wanapigana. Ngoja tuone shetani yupi atashinda...

Siku za mwisho hizi tutaona mengi!!!!

Anonymous said...

Mwingira Mwingira Mwingira
Wewe ni nani hado umtangazie binadamu mwenzio KIFO? Nina mashaka na utumishi wako? Badala ya kusimama mbele ya madhabahu na kuropoka maneno makali hivyo ungeingia kwenye maombi umuombee babu ili aache kuwadanganya watu(kama ni kweli) na pia amuombe Mungu awafu gue macho ya kiroho watu ili waone ukweli wa mambo. Pamoja na hayo alipaswa awafundishe watu kweli ili iwaweke huru. Kuongea ongea tu bila kufanya lolote hakumsaidii yeye mwenyewew Mwingira, babu wala watu wanaoenda huko. Zaidi sana watu wanamwona Mwingira kama ana chuki na Babu tu.

Mwingira kwakweli hapo amechemsha kabisa; anafanya mambo kama mtaifa asiyejua maandiko? Watu wanamshangaa kabisa! Mbona alivyosema muumini wa kanisa lake atakayeenda kwa babu atakufa watu wameenda na hawajafa na kwanini awatishe watu badala ya kuwafundisha kweli. Kwa sababu mtu ataogopa kwenda kwa babu kwa sababu askofu wake kasema akienda atakufa; kitu ambacho si sahihi. Watu wanatakiwa wasiende kwa sababu wanaijua kweli juu ya tiba hiyo.

Mwingira funguka!

Anonymous said...

huko ni kufirisika kiimani, pengine ni kweli kuwa huduma yake inakwenda minyume na maandiko yake; Je hata kama ni askofu ni askofu wa aina gani huyu? nafikiri angeanza kwanza kutoa boriti ndani ya jicho lake ndipo atoe kibansi katika jicho la babu;
ama kweli tunaangamia kwa kukosa maarifa; Mungu amfunue macho ili aweze kuhubiri kweli inayotakiwa mbele ya Mungu Amina