Audio ya Sinema ya Yesu Katika Kisukuma
  
Audio ya Sinema ya Yesu Katika Kiswahili

Tuesday, August 23, 2011

Jambo Hili Halikunifurahisha !!!

Picha hii iko HAPA

Leo wakati natafuta nyimbo za Rose Muhando na Bahati Bukuku katika Youtube, nimekutana na mambo ya ajabu. Watu wameamua kuweka "mihadhara" yenye kutetea dini ya Kiislamu kwa kutumia majina ya waimbaji mashuhuri wa injili kama Rose Muhando, Bahati Bukuku na wengineo (mf. tazama HAPA).

Video ina jina la Rose Muhando lakini ukibofya unapelekwa kwenye video inayoonyesha mihadhara ya kitoto kati ya Uislamu na Ukristo - mihadhara ambayo lengo lake hasa mimi huwa silielewi japo kuna kipindi ilikuwa imejikita sana kule nyumbani.  Kwa kawaida katika mijadala hii Ukristo huwa unashambuliwa sana, Biblia hupotoshwa na kutafsriwa nje ya mandhari na muktadha wake; na Uislamu hushadidiwa kuwa ndiyo dini ya kweli na mwanzilishi wake kuwa ndiye hasa mtume wa mwisho aliyefunga kazi. Daima mwamba ngoma huvutia kwake ati!

Hata hivyo ukisikiliza na kufuatilia vizuri mijadala hii ni wazi kwamba hoja nyingi zinazotolewa zimeegemea katika mihemko, hazina nguvu, zimejaa jazba, hazina umakinifu na hazijachujwa vizuri. Unaweza hata kupata fununu kuhusu kiwango cha elimu-dunia cha watoa mihadhara hawa na wasikilizaji wao ambao wengi wao kazi yao kubwa ni kushangilia tu!

Sina ugomvi na Waislamu na mtume wao wala dini zingine na waanzilishi wao kwani naamini kwamba ni uhuru wa kila mtu kuamini dini yo yote anayotaka. Hata hivyo huwa nakerwa na watu wanaosimama kidete na kuanza kushambulia dini zingine hata ikibidi kwa kutumia matusi (ya kitashtiti) na udogoshaji. Historia inaonyesha kwamba mashambulizi ya aina hii mara nyingi yana madhara makubwa kijamii hasa upande mmoja unapokuwa hauna subira na uvumilivu. Ndiyo maana tukaonywa kwamba kama unaishi katika nyumba yenye vioo basi kamwe usishabikie mchezo wa kurusha mawe. Dini !!!

Ati,  Ukristo ndiyo dini ya kweli? Uislamu ndiyo dini ya kweli? Uhindu je? Dini zingine nazo? Vipi kuhusu dini zetu za Kiafrika tulizokuwa nazo kabla ya ujio wa Waarabu na Wazungu katika mwambao wa Afrika Mashariki? Kwa kuwa dini hizi tumezichanganya na dini tulizoletewa, je hizi nazo ni za kweli?

Ukiona jamii inaanza kubetuana kwa kutumia misingi ya udini, basi jua kwamba jamii hiyo inacheza na moto na inakoelekea si kwema! Na watu wanaoendekeza na kushabikia haya mambo ya udini (wakiwemo hawa watoa mihadhara uchwara) ni watu wa kuogopwa kama ukoma. Mwenye masikio na asikie !!!

No comments: